• PRO
  • 02 Feb 2026
  • Iringa

Maadhimisho ya Siku ya Sheria - Tanzania

Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (RUCU) kimeungana na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa katika kuadhimisha Siku ya Sheria Nchini, tukio lililofanyika katika viunga vya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, likilenga kuhimiza na kuimarisha utawala wa sheria, haki na uwajibikaji katika jamii.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, mahakama, vyombo vya ulinzi na usalama, taasisi za elimu ya juu, wanasheria, viongozi wa dini pamoja na wadau wa haki, huku Mgeni Rasmi akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri Denice James.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa, Dunstan Ndunguru, alisema Mahakama ya Tanzania itaendelea kusimamia haki kwa uadilifu, uhuru na bila woga wowote, akisisitiza kuwa utawala wa sheria ni mhimili muhimu wa amani, ustawi wa jamii na maendeleo endelevu ya taifa.

“Mahakama imepewa dhamana ya kikatiba ya kutoa haki bila hofu, upendeleo wala shinikizo. Haki ya kweli ndiyo msingi wa maendeleo ya kudumu, na tutaendelea kuitumikia jamii kwa misingi hiyo,” alisema Jaji Ndunguru.

Katika maadhimisho hayo, Kitivo cha Sheria - RUCU kilitambulika kama mdau muhimu katika maendeleo ya elimu na mafunzo ya sheria nchini. RUCU ni chuo kinachotoa programu za sheria kuanzia ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada ya Kwanza, Shahada za Uzamili hadi Uzamivu (PhD), na kimekuwa kikishirikiana kwa karibu na Mahakama katika kuwapatia wanafunzi wa sheria fursa za mafunzo kwa vitendo kupitia mafunzo ya kimahakama na uzoefu wa kazi za kitaaluma.

Ushirikiano huo umeelezwa kuwa unalenga kuwaandaa wanafunzi wa sheria kuwa wataalamu wenye uelewa wa vitendo, maadili ya taaluma na misingi ya utoaji haki, sambamba na mahitaji halisi ya mfumo wa haki nchini.

Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Kheri Denice James, alipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu, na akawashukuru na taasisi mkoani Iringa kwa mchango wao katika kuimarisha utawala wa sheria nchini.


Source: External

Advertisement